Searching...
Image and video hosting by TinyPic
20 December 2014
Saturday, December 20, 2014

Okwi nje mechi na Kagera Sugar



Na Oscar Oscar Jr

Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda na klabu ya Simba, Emmanuel Okwi anatarajiwa kuikosa mechi ya mzunguko wa nane ya ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Kagera Sugar ambayo imepangwa kuchezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Desemba 26 kutokana na mchezaji huyo kuwa kwenye mapumziko ya ndoa huko kwao.

Habari zilizotufikia mshambuliaji huyo ambaye amezaliwa mwaka 1992, jana alitarajia kufunga ndoa nyumbani kwao nchini Uganda na hivyo amepewa muda wa mapumziko kabla ya kurejea uwanjani na kuhakikisha Simba inapata matokeo ya ushindi na kufufua mbio za kutwaa ubingwa ambao klabu hiyo imeukosa kwa misimu kadhaa sasa.

Kagera Sugar ambao wanakamata nafasi ya tano na pointi 10, tayari wanaonekana kuwa timu tishio kwani wameshafanikiwa kuwafunga Yanga na kutoka sare na vinara wa ligi hiyo, timu ya Mtibwa Sugar. Simba msimu uliopita ilishindwa kupata ushindi kwenye mechi zote mbili ambazo walikutana na Kagera Sugar.

Tayari imebainishwa kuwa mshambuliaji mpya wa Simba kutoka klabu ya Gor Mahia, Danny Sserunkuma amekabidhiwa mikoba ya kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kabla ya Okwi kurejea na kuongeza nguvu. 

Sserunkuma ambaye aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu nchini Kenya msimu uliopita, amebeba matumaini makubwa kwa wana Msimbazi. Mbali ya ufungaji bora, amewahi pia kushinda tuzo ya  mchezaji bora wa mwaka nchini Kenya akiwa ndiye mchezaji wa kigeni wa kwanza kuwahi kufanya hivyo.

Baada ya mechi saba za awali, Simba wamejikuta wakikamata nafasi ya saba baada ya kushinda mechi moja na kutoa sare mara sita na sasa, wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na alama tatu kwenye kila mchezo watakaoshuka dimbani. 

Tofauti za kiuuongozi, mtafaruku wa mashabiki wao waliojulikana kwa jina la UKAWA, sasa wanaonekana kuwa kitu kimoja na hii ni dalili nzuri kwa timu hiyo yenye maskani yao mtaa wa Msimbazi ndani ya jiji la Dar es salaam.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!