Searching...
Image and video hosting by TinyPic
4 December 2014
Thursday, December 04, 2014

NIONAVYO MIMI: SOKA LETU LINAONGOZWA NA WANAMUZIKI



Na Oscar Oscar Jr


Ukizungumza na watu wa zamani, wanakwambia muziki wa zamani ulikuwa bora kuliko Bongo Flava ya leo. Ukiuliza kuhusu Elimu, utaambiwa mfumo wa zamani ulikuwa bora kuliko huu wa sasa na hata ukiuliza kuhusu wachezaji wa soka, utaambiwa zamani walikuwa bora kuliko hawa wa leo.


Zamani muziki haukuwa unalipa, soka halikuwa linalipa, filamu hazikuwa zinalipa lakini vipaji vilionekana. Tasnia hizi hazikushirikisha kila mtu. Aliyeuweza muziki kweli kweli, ndiye aliyejiunga. Aliyeuweza mpira hasa, ndiye aliyeucheza. Wengine walikubali kuwa watazamaji na maisha yakaendelea.


Tanzania inaonekana kufaulu zaidi kwenye maeneo ambayo hayahusishi fedha. Wakati Elimu inatolewa bure, ubora ulipanda.
Wakati muziki hauingizi fedha nyingi, ubora ulipanda na hata wakati mpira unachezwa bure, kiwango pia kilipanda. Tatizo ni fedha?


Ukitangaza leo hii unahitaji vijana watano wenye uwezo wa kucheza Filamu, watakuja elfu kumi. Ukihitaji vijana kumi wenye uwezo wa kuimba, watakuja elfu 20. Ukihitaji wachezaji wa soka kumi, watakuja elfu hamsini na hata ukihitaji viongozi wa soka watatu, nao watakuja elfu hamsini.


Baada ya kuona fedha inapatikana kwenye Bongo Flava, vijana wengi wanataka kuwa wasanii. Baada ya kuona mpira unalipa, kila mtu anataka kucheza. Baada ya kuona Uongozi wa soka unalipa, kila mtu anataka kitengo. Tatizo ni fedha?


Vijana wengi hapa nchini hasa waliobahatika kupata Elimu ya Chuo kikuu, wanatamani kuwa wabunge. Unadhani ni kwasababu wanafahamu matatizo ya wananchi? hapana.


Wanajua ukiupata Ubunge, maisha umeyapatia. Wanajua ukiupata Ubunge umasikini ndiyo bai bai! Upo uwezekano mkubwa kuwa, hata bunge la zamani nalo lilikuwa bora kuliko hili lililojaa kina "Ashki Majinuni"


Mpira wa nchi yetu kwa sasa unahama kutoka kuwa burudani kwenda kuwa biashara lakini, viongozi wa soka letu wao wanahama kutoka kuwa biashara kwenda kuwa burudani! Tutafika kweli?

Ukitazama namna uendeshwaji wa soka letu hapa nchini, kuna muda inaonekana kabisa wanaoongoza sio watu wa soka. Ukitazama utendaji wa kamati ya Miss Tanzania, unagundua kabisa kuwa imejaa watu ambao sio wenye taaluma ya ulimbwende.

Au watu wa Ulembwende ndiyo wako kwenye soka letu na wa soka wako kwenye Ulimbwende? au watu wa Muziki wako kwenye soka na watu wa soka wako kwenye Muziki? au watu wa filamu wako kwenye soka na wa soka wako kwenye Filamu? sijapata jibu.

Hii yote ni kwa sababu watu wanatafuta pesa. Ili usajiliwe unahitaji mtu wa kukushika mkono. Ili uitwe timu ya Taifa sio kipaji na uwezo tena, unahitaji mtu akushike mkono. Ili uwe kiongozi wa soka, sio uwezo bali uwe na watu wa kukushika mkono!

Baada ya wizara ya Elimu hapa nchini kuonekana ndiyo mahali pakee kwenye ajira ya uhakika, wahasibu wamekuwa waalimu, wahandisi wamekuwa waalimu na kila mtu aliyekosa ajira ya taaluma yake, amekimbilia kwenda kufundisha shule zetu. Matokeo si mnayaona?

Kupeana ulaji pale TFF, kushindwa kuandaa michuano ya vijana, kufungua dirisha la usajili baada ya mechi saba tu za ligi kuu na mengine mengi, huenda ni matokeo ya soka letu kuongozwa na wanamuziki.

1 comments:

  1. Soka letu limekosa mwelekeo,hii ni kutokana na kukosa viongozi halisi wa soka,
    Tumekuwa na viongozi wenye kuongoza kwa hisia na mizuku,soka halitaki hivyo soka linaueledi wake bhana,soka ni zaidi ya kucheza,maandalizi mabovu,viongozi wanafikiria kesho waseme nn ili wacgiwe then mpira upande hiyo ni ndoto.
    Vunja kila kitu tuanze upya japo dawa ni chungu lkn ndy inayoponyesha hainabudi tuinywe tuu...

    ReplyDelete

 
Back to top!