Searching...
Image and video hosting by TinyPic
20 December 2014
Saturday, December 20, 2014

Hatimaye kimeeleka kwa Azam.


Na Oscar Oscar Jr

Mabingwa watetezi wa Tanzania bara timu ya Azam ambayo imeweka kambi ya siku 10 nchini Uganda, hatimaye jana waliweza kuibuka na ushindi wao wa kwanza kwenye ziara hiyo baada ya kupata na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya timu ya Vipers inayoshiriki ligi kuu nchini Uganda.

Kabla ya mchezo huo wa jana, Azam walikuwa tayari wameteremka mara mbili dimbani na kujikuta wakichezea vichapo mechi zote ambapo, mchezo wao wa kwanza walilala kwa mabao 3-2 kutoka kwa timu ya SC Villa kabla ya kuchezea tena kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa URA.

Ushindi huo wa jana utakuwa umeibua ari mpya kwa wachezaji na benchi la ufundi hasa ukizingatia kuwa, baada ya ligi ya Tanzania bara kuanza, watalazimika kukutana na timu ya Yanga ambayo mchezo wa awali wa ngao ya jamii Azam alifungwa mabao 3-0.

Magoli ya Azam kwenye mchezo huo wa jana yalifungwa na mchezaji bora wa ligi kuu msimu uliopita, Kipre Tchetche ambaye alifunga mara mbili huku bao lingine likifungwa na Hamis Mcha. 

Azam wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kushuka dimbani mara saba na kuambulia alama 13 ambazo ni sawa na walizopata Yanga na kinachowatofautisha ni magoli ya kufunga na kufungwa ambapo Yanga anashika nafasi ya pili.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!