Searching...
Image and video hosting by TinyPic
7 November 2014
Friday, November 07, 2014

Wachezaji wa Azam kupigwa bei dirisha dogo.




Na Oscar Oscar Jr

Kupitia Gazeti la michezo la Champion la leo, kuna habari kuhusu timu ya Azam, kuwapiga bei wachezaji wake watatu ambao ni golikipa Mwadini Ally, beki Shomary Kapombe na mshambuliaji Kipre Tchechte. 

Azam kwa sasa wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara, mara baada ya kushuka dimbani mara sita na kuambuliaji alama 10 pekee.

Kipre Tchetche ambaye  aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu Tanzania msimu wa 2012/2013, siku za hivi karibuni amekuwa akiripotiwa kutokuwa pamoja na kambi ya timu hiyo kutokana na kuwa na matatizo yanayoihusu familia yake nchini Ivory Coast.

Wakati timu hiyo ikipokea vichapo kutoka timu za JKT Ruvu na Ndanda Fc, Kipre hakuwepo na tayari kupitia website ya timu hiyo, kuna habari za mchezaji huyo kuukosa pia mchezo wao unaofuata dhidi ya Coastal Union kutokana na kutorejea kutoka kwao nchini Ivory Coast.

Beki Shomary Kapombe ambaye alisajiliwa kutoka nchini Ufaransa, naye ametajwa kuwekwa sokoni kutokana na madai ya kushuka kwa kiwango chake huku kukiwa na taarifa pia za kumuuza kipa wao Mwadini Ally. 

Azam kwa sasa inamtumia kipa Aishi Manula na kama Mwadili ataondoka kwenye klabu hiyo, ni wazi kuwa timu hiyo itahitaji kununua kipa mwingine.

Wachezaji hao wote, wanamikataba na timu hiyo na taarifa zinaeleza kuwa, Azam wakotayari kuwauza kwa timu yoyote inayowahitaji ndani au nje ya nchi. Tayari kuna habari kuwa, Kipre Tchetche anaweza kuelekea nchini Malaysia au Kenya kwenye klabu ya Sofapaka.

Jumamosi hii timu ya Azam itashuka dimbani kuumana na Coastal Union kwenye muendelezo wa michezo ya ligi kuu, mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Chamazi Complex, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam. 

Coastal Union wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara wakiwa na alama 11 huku Azam, wakitaka kuutumia mchezo huo kujiimarisha kutokana na kupoteza michezo miwili mfululizo.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!