Searching...
Image and video hosting by TinyPic
28 November 2014
Friday, November 28, 2014

Uchambuzi: Southampton vs Manchester City siku ya Jumapili.


 Na Oscar Oscar Jr

Gumzo kubwa kwenye ligi kuu Uingereza wikend hii, ni kwenye mchezo wa siku ya Jumapili ambao utawakutanisha Southampton dhidi ya bingwa mtetezi, Manchester City kwenye dimba la St. Marry. 

Southampton wako kwenye nafasi ya pili huku wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja nyumbani msimu huu, watakutana na Manchester City ambao wanaonekana kurejea katika ubora wao.

Nguzo kubwa ya mafanikio wanayoyapata Southampton ni kuimarika kwa safu yao ya Ulinzi kwani mpaka sasa, wameruhusu mabao sita pekee. Saints wanaonekana kufanya vizuri zaidi nyumbani kwani katika pointi 18, wao wamepata 16.

Kipa Fraser Foster ameonyesha kiwango bora na kwasasa, ndiye anayeshikilia ufalme wa kukaa langoni mechi saba bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Mechi hii itakuwa ni kipimo tosha kawa vijana wa kocha Ronald Koeman kwa sababu, Saints wanaonekana kucheza na kupata ushindi pale wanapocheza na timu ambazo msimu uliopita, zilimaliza juu ya nafasi ya saba. 

Ushindi dhidi ya Manchester City, utaanza kuthibitisha mwelekeo wa timu hiyo kujaribu kumaliza kwenye nafasi ya nne msimu huu huku endapo Man City watapata pointi tatu, safari ya kumkimbiza Chelsea itakuwa imeanza rasmi.

Sergio Aguero ambaye anaonekana kuwa kwenye ubora wa hali ya juu, anaonekana kufanya vizuri zaidi pale anapotumika kama mshambuliaji wa mwisho tofauti na vile alivyokuwa anacheza nyuma kidogo ya Eden Dzeko. 

Alionekana kuisambaratisha Spurs kwa kufunga mabao mnne na hivi karibuni, amefanikiwa kupiga Hat-Trick dhdi ya Bayern Munich kwa kutumiwa kama mshambuliaji wa mwisho.

Dusan Tudic kwa upande wa Southampton, anaonekana fundi sana katika kupika pasi za mwisho lakini, sio mzuri kwenye kuanzisha mashambulizi. 

Saint wanamtegemea zaidi Steven Davies ambaye anaonekana kuwa kwenye hati hati ya kucheza mechi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa, hata mchezo wa sare ya bao 1-1 dhidi ya Aston Villa hakuweza kucheza kutokana na majeruhi.

Man City waliwakosa, Viungo Yaya Toure na Fernandinho ambao walikuwa na adhabu za kucheza mchezo wa klabu bingwa Ulaya lakini, mafundi hao wa dimba la kati wanatarajia kurejea kwenye mchezo dhidi ya Saints huku Toure akionekana kuanza taratibu kurejea kwenye ubora wake baada ya wiki iliyopita, kufanya vizuri dhidi ya Swansea City na kuipatia timu yake bao la ushindi.

Saint wanaonekana kukabia kwa juu, kitu ambacho kimewafanya washambuliaji wa timu pinzani kuotoa mara nyingi wanapocheza na Southampton kuliko timu yoyote kwenye ligi lakini, timu hiyo haijakutana na washambuliaji wa aina ya Aguero msimu huu.

Fraser Foster kwenye mchezo dhidi ya Aston Villa alifanya kosa kipindi cha kwanza kwa kutokuwa na maamuzi sahihi kitu kilichomfanya Gabby Agbonlahor afunge bao jepesi. Morgan Schneiderlin na Victor Wanyama, wanahitajika pia kuwa kwenye ubora wao ili kuimudu vita ya Toure na Fernandinho.

Kwa upande wa Joe Hart, kama kawaida ameendelea kuwa na tatizo la maamuzi na hili lilithibitishwa na namna alivyokubali magoli mawili ya Bayern Munich kirahisi. 

Namna alivyojipanga wakati Xaib Alonso anapiga mpira wa adhabu na goli la Robert Lewandowski, yanadhihirisha namna kipa huyo anavyojipanga vibaya langoni. 

Ulinzi wa Manchester City, siku zote unategemea ubora wa Vincent Kompany. Graziano Pelle ni aina ya mshambuliaji ambaye anaonekana kuwa na shabaha pale anapopata nafasi. 

Martin Demichellis au Eliaquem Mangala ambao mmoja atacheza na Kompany, ni lazima awe kwenye ubora ili kuepuka madhara yanayoweza kuletwa na mshambuliaji huyo wa Saints ambaye ndiye kinara wa timu yake kwa mabao.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!