Searching...
Image and video hosting by TinyPic
7 November 2014
Friday, November 07, 2014

Uchambuzi: Manchester United vs Crystal Palace


Na Chikoti Cico

Ligi kuu ya Uingereza itaendelea kushika kasi tena wikendi hii huku kwenye kiwanja cha Old Trafford nyumbani kwa mashetani wekundu, timu ya Manchester United itaikaribisha Crystal Palace huku kila timu ikitafuta alama tatu muhimu.

Manchester United ambao wanashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi nchini Uingereza wakiwa na alama 13 baada ya michezo 10 wanatarajia kuingia kwenye mchezo huo kutafuta ushindi wake wanne toka msimu kuanza na kuendelea kupigana kuingia kati ya timu nne za juu (Top 4) kwenye msimamo wa ligi.

Kocha wa Manchester United Luis Van Gaal bado anasumbuliwa na wachezaji wengi majeruhi hasa sehemu ya ulinzi, United watawakosa Radamel Falcao na mabeki Jonny Evans, Marcos Rojo, Phil Jones ambo ni majeruhi huku Rafael akiwa na hatihati ya kutokuanza pia itamkosa Chris Smalling anayetumikia adhabu.

Kwa kuwakosa mabeki hao kiungo wa ulinzi wa Manchsester United Michale Carrick anatarajiwa kucheza kama beki wa katikati akishirikiana na kati ya Tyler Blackett ama Paddy McNair.

Wakati huo huo takwimu zinaonyesha katika mechi 12 zilizopita nyavu za United hazijatikiswa mara mbili tu (clean sheet) huku pia United wakiongoza kwa wachezaji kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye msimu wa 2014/15 mpaka sasa wachezaji watano wameonyeshwa kadi nyekundu.

Kikosi cha Manchester United kinaweza kuwa hivi: De Gea; Valencia, Carrick, McNair, Shaw; Fellaini, Blind; Januzaj, Rooney, Di Maria; Van Persie

Kwa upande wa Crystal Palace hali sio nzuri kwani mpaka sasa wamepoteza mechi nne zilizopita hivyo kupelekea kushuka mpaka nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama tisa tu. Hivyo wanahitaji kupigana kupata alama tatu muhimu dhidi ya Manchester United.

Kocha wa Crystal Palace Neil Warnock atamkosa nahodha wake Mile Jedinak aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Sunderland, naye Wilfred Zaha hatacheza kwa kuwa yuko Palace kwa mkopo kutoka United. Kurejea kwa Damien Delaney aliyekuwa majeruhi kunatarajiwa kuiongezea nguvu Palace kwenye mchezo huo.

Takwimu zinaonyesha Palace wameshindwa kufunga katika mechi nane kati ya 10 zilizopita walizocheza na United huku pia katika michezo mitatu iliyopita miwili kati yao mchezaji wa Palace alionyeshwa kadi nyekundu walipocheza na United.

Kikosi cha Crystal Palace kinaweza kuwa hivi: Speroni; Ward, Dann, Delaney, Kelly; Puncheon, McArthur, Ledley, Bolasie; Chamakh, Campbell

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!