Searching...
Image and video hosting by TinyPic
18 October 2014
Saturday, October 18, 2014

Uchambuzi: Yanga 0-0 Simba


Na Oscar Oscar Jr

Mchezo wa Yanga na Simba umemalizika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kwa timu hizo kwenda sare pacha huku, Simba wakionekana kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa kuliko Yanga, hususani kwenye kipindi cha Kwanza. 

Kipindi cha pili Yanga waliongeza nguvu na kuimarika zaidi hasa pale Said Ndemla na Jonas Mkude wote walipotolewa kutokana na majeruhi.

Yanga walionekana kuwa imara kwa kushambulia kupitia upande wa kulia ambako, Mrisho Ngassa alicheza dhidi ya beki wa Simba Mohamed Hussein, maarufu kama Tshabalala. 

Tshabalala alionekana kupanda mara kwa mara kuongeza mashambulizi ya Simba na kujikuta mara kadhaa, akizidiwa ujanja na Ngassa ambaye ana  kasi kuliko beki huyo.

Takwimu zinaonyesha Simba kumiliki mpira kwa asilimia 51 dhidi ya Yanga ambao wamepata asilimia 49. Tofauti hii sio kubwa sana na hii ni kwa sababu, baada ya viungo wawili wa kati walioanza kwa upande wa Simba kutolewa, Yanga walinufaika na mabadiliko hayo.

Mabadiliko ya kocha Maximo kumpunzisha Haruna Niyonzima, nadhani haikuwa sahihi. Alipaswa kuwapumzisha Andrey Coutinho na Hassani Dilungu huku Niyonzima akimrejesha dimba la juu na kuwaongeza Simon Msuva na Hamis Kiiza kumsaidia Jaja.

Bado sielewi ni kwa nini Simon Msuva anaendelea kukaa benchi! Yanga hii ya Maximo haishambulii kama ile ya kocha Hans Van Pluijm, ni bora Maximo akamuanzisha Ngassa na Msuva kisha baada ya ushindi, ndiyo arudi kuzuia. 

Yanga hii, inazuia zaidi kuliko kushambulia na takwimu zinaonyesha leo walikuwa na mashuti sita tu, matatu yalilenga goli na mengine nje.

Bado ni mapema sana kumwagia sifa golikipa kijana wa Simba, Peter Manyika Jr aliyecheza mechi ya leo ingawa ameonyesha hali ya kujiamini. Hassan Isiaka na Joseph Owino, walimpatia ulinzi wakutosha. Hakuwa na kazi kubwa sana hivyo haikuwa kazi ngumu kwake kucheza dakika 90 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Emmanuel Okwi ni mchezaji bora wa mchezo huu kwa mujibu wa mtandao huu. Alikwa mwiba mkali sana dhidi ya walinzi wa Yanga muda wote alipokuwa na mpira mguuni na hii, iliwafanya Yanga kucheza madhambi mara nyingi (13) kuliko Simba.

Bado sijafahamu ni kwa nini Amis Tambwe aliwekwa nje kwa upande wa Simba. Kama ni kwa sababu za kitabibu sawa ila kama kocha Patrick Phiri atakuwa amemuweka nje kwa sababu za kiufundi, nadhani atakuwa amemkosea heshima. Mchezo kiujumla, ulikuwa wa kawaida sana.



0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!