Searching...
Image and video hosting by TinyPic
24 October 2014
Friday, October 24, 2014

Uchambuzi: Sunderland vs Arsenal


Na Chikoti Cico

Baada ya kubugizwa kwa jumla ya magoli 8-0 na Southampton timu ya Sunderland inarejea tena dimbani kuikaribisha timu ya Arsenal kwenye mchezo wa ligi kuu ya Uingereza utakaopigwa kwenye uwanja wa Stadium of Light nyumbani kwa Sunderland.

Huku wakishika nafasi ya 17 wakiwa na alama nane kwenye msimamo wa ligi, Sunderland wanahitaji kupigana kufa na kupona ili kutafuta alama tatu muhimu dhidi ya Arsenal na kuweza kuamsha matumaini mapya ya kutokushuka daraja.

Pia Sunderland watakuwa na nia ya kuwafuta machozi mashabiki wao waliopata aibu ya kufungwa magoli nane kwenye mechi iliyopita dhidi ya Southampton.

Kocha Gus Poyet ambaye mpaka sasa hajapoteza mchezo wowote wa ligi nyumbani huku akiwa amecheza michezo minne na kushinda mchezo mmoja na kutoka sare michezo mitatu.

Kocha huyo atawakosa mabeki Sebastian Coates na Billy Jones huku pia akiwakosa viungo Ricky Alvarez,na Emanuele Giaccherini ambao wote ni majeruhi.

Takwimu zinaonyesha Sunderland toka kuanza msimu wa mwaka 2010-11 mpaka sasa, inaongoza kwa kujifunga magoli mengi. Imejifunga jumla ya magoli 15, huku pia kati ya michezo 21 iliyopita dhidi ya Arsenal kwenye ligi, imeshinda mchezo mmoja tu.

Kikosi cha Sunderland kinaweza kuwa hivi: Mannone; Reveillere, Brown, O'Shea, Van Aanholt; Cattermole, Larsson, Rodwell; Johnson, Wickham, Fletcher

Timu ya Arsenal wao wataendela kuwakosa Laurent Koscielny, Mesut Ozil, David Ospina, Yaya Sanogo, Abou Diaby, Olivier Giroud na Mathieu Debuchy ambao wote ni majeruhi huku kiungo Jack Wilshere akitumikia adhabu baada ya kuonyeshwa jumla ya kadi tano za njano.

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger anatarajia kutafuta ushindi wake wa pili ugenini kwani mpaka sasa katika mechi nne timu ya Arsenal ilizocheza ugenini imeshinda mchezo mmoja, imetoka sare michezo miwili na kufungwa mchezo mmoja.

Arsenal inaweza kuweka rekodi mpya kwenye historia ya ligi kuu ya Ungereza kwa kuwa timu ya pili baada ya Manchester United kufikisha magoli 1500 huku ikihitajika kufunga magoli mawili tu kuweza kuifikia rekodi hiyo.

Kikosi cha Arsenal kinaweza kuwa hivi: Szczesny, Chambers, Mertesacker, Monreal, Gibbs, Flamini, Oxlade-Chamberlain, Ramsey, Cazorla, Sanchez, Welbeck.

Takwimu zinaonyesha katika michezo 134 ya Ligi kuu ya Uingereza ambayo Sunderland na Arsenal zimekutana Arsenal imeshinda michezo 52 huku Sunderland ikishinda michezo 44 na wametoka sare michezo 38.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!