Searching...
Image and video hosting by TinyPic
11 April 2014
Friday, April 11, 2014

NIONAVYO MIMI:WAACHENI LIVERPOOL WAENDELEE KULA UJANA.


Na Oscar Oscar Jr
+255789784858

Kuna muda unakutana na kijana ameishusha kabisa suruali yake chini ya kiuno,unabaki umepigwa na mshangao! wakati wewe ukiendelea kumshangaa,mwenzio hana kabisa habari.Ni jambo la kawaida kabisa kukutana na binti ambaye robo tatu ya maungo ya mwili wake yako nje kutokana na mavazi aliyovaa,lakini mwenyewe ndiyo kwanza anazidisha mikogo.Raha jipe mwenyewe bwana.Ukijifanya unataka kumpa ushauri,atakujibu kwa kifupi tu "niache,nakula ujana"  utakuwa na swali tena? hapana,utaendelea tu na shughuli zako.

Wakati msimu wa 2013/2014 wa ligi kuu Uingereza unaanza,ilikuwa ni vigumu sana kuamini kama timu ya Liverpool muda huu itakuwa juu ya kilele cha "Mlima Kilimanjaro" kwenye msimamo wa ligi hiyo,juu ya Chelsea,Man City na watoto wa London,Arsenal.Ukimtazama kocha Brendan Rodgers kisha,ukamlinganisha na ukubwa wa timu ya Liverpool,unagundua kabisa,ilikuwa ni Suruali iliyomzidi kiuno.Kwa namna yoyote ile,alitakiwa kuivaa kwa kutumia ama mkanda,kwenda kuipunguza kwa fundi au kuvaa "mlegezo". Pamoja na haya yote,Brendan Rodgers hakutaka kumjibu mtu,aliamua kuanza kula ujana na wanae wa Liverpool.

Ukitazama ukubwa wa kikosi chao,unagundua kabisa kwamba ni kidogo sana.Sio jeshi ambalo linaweza kucheza mechi za FA,Capital one na kupigania nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi kuu ya EPL.Kabla ya msimuu huu kuanza,ilikuwa ni vigumu sana kuamini kama Jonathan Patrick Flanagan,atakuja kuwa moja ya mabeki bora wa majogoo hao wa jiji la Liverpool.

Timu za Arsenal,Chelsea na Manchester City ndizo zilizokuwa zinapewa nafasi kubwa sana ya kutwaa Ubingwa ingawa,mpaka sana,Arsenal ameishiwa pumzi.Safari imekuwa ni ndefu kuliko nauli yao,wamemuomba kondakta awashushe wakapiganie kuipata nafasi ya nne ambayo wameizoea! Bado Chelsea na Manchester City wananafasi ya kutwaa taji hili ingawa,Liverpool wameamua kumkimbiza mwizi kimya kimya.


Msimu huu Liverpool,wamepoteza alama kwenye michezo miwili tu wanapokuwa uwanja wao wa nyumbani,pale Anfield.Walifungwa na Southampton bao 1-0 na kutoka sare ya mabao 2-2 na timu ya Aston Villa.Arsenal walifungwa 5-1,Everton walifungwa 4-0,Spurs 4-0 kwa kifupi tu,unaweza kusema Liverpool wanakula ujana.

Ni vigumu kujua siri ya mafaanikio ya Liverpool na ukiona jambo limefikia hapo,ndiyo mwanzo wa kuanza kujiuliza maswali mengi kuliko majibu unayoyapata!.
Ni kwa sababu ya mechi chache? Hii kidogo inaweza kunihamasisha. Katika timu saba za juu kwenye msimamo wa EPL, ni Liverpool na Evaton tu ambao wamekuwa na mechi chache. Baada ya Liverpool kutolewa mapema kwenye kombe la FA na Capital one, nguvu zao zote waliwekeza kwenye ligi.Liverpool wanacheza mechi moja kwa wiki, kwa hali ya kawaida wachezaji wao wanapata muda mwingi sana wa kupumzika tofauti na wenzao ambao wamefika mabli kwenye michuano ya Ulaya na makombe ya FA na Capita One.

Ni ubora wa wachezaji? Kama nivyosema hapo awali, Liverpool haikuwa na wachezaji wengi ambao ungeweza kuwaita bora kabla ya msimu kuanza ukimwondoa Steven Gerrard na Luiz Suarez ambao ubora wao kwa muda mrefu umekuwa ni ule wa kiwango cha dunia. Raheem Sterling hakuwa na wakati mzuri sana msimu uliopita, lakini kwa sasa ni mmoja kati ya viungo washambuliaji bora kwenye EPL. Ilikuwa ngumu sana hata kwa kocha mkongwe kama Sir Alex Ferguson kumkubali Jordan Henderson kama kiungo bora lakini kwa sasa, nadhani mzee Fergie anaisoma namba kimya kimya. Anachokifanya golini Simon Mignolet, sidhani kama kuna mtu anamkumbuka tena golikipa Pepe Reina. Una swali? acha tu picha liendelee.

Kuna msaada wa waamuzi? Kwa muda mrefu sana tumeshuhudia klabu ya Manchester United ikiwa katika ubora wake na kulikuwa na baadhi ya maamuzi ambayo yalikuwa yanawabeba. Kwa sasa hali nitofauti, picha limegeukia mtaa wa saba kwa majogoo wa jiji Liverpool. Ukimgusa tu Luiz Suarez, wanapata penati na kaka mkubwa Gerrard hafanyi makosa. Ukithubutu hata kumnusa Daniel Sturridge ili ujue manukato aliyojipulizia siku hiyo, wanapewa penati nyingine; jamani Liverpool msitufanyie hivyo.Lakini, ukiona timu inapewa penati nyingi maana yake ni kwamba, wanafika sana kwenye eneo lako. Poa tu, kama vipi acha tu picha liendelee.

Ni ubora wa kocha? Kuna muda pia najiuliza swali kama hili kwa sababu, Brendan  Rodgers ndiye kocha aliyeifanya timu ya Swansea City kuitwa jina la "Swansealona" kutokana na soka la tiki-taka ambalo ni maarufu kwa watoto wa Katalunia, timu ya Barcelona. Liverpool ya sasa inacheza soka la kasi huku wakipiga wastani wa pasi zaidi ya 500 kwenye kila mechi. Steven Gerrard kambadilisha na kumpa jukumu la kuzuia zaidi badala ya kushambulia, Raheem Sterling mechi ya hivi karibuni dhidi ya Westham, alibadilishwa nafasi na kucheza kama kiungo wa kati. Mwendo ukawa ni ule ule "mchibuyu" Rodgers, unataka kuifanya Liverpool nayo iwe "Liverpoolona"?

Ni ubora wa Sturridge na Suarez? kuna muda mpira naufananisha na somo la Hisabati.Kama mbili kujumlisha tatu jibu lake ni tano,hata ufanye nini,itaendelea kubaki kama ilivyo.Kuna uwezekano ukawa haumpendi Luiz Suarez ama kwa chuki zako binafsi au wivu unaokusumbua lakini ukweli utabaki pale pale. Jamani ni Mafia, Komandoo,mbishi sugu kila anapokuwa mbele ya lango tayari ana magoli 29, katengeneza mengine 11 katika michezo 28 tu aliyocheza msimu huu. Kumchukia Suarez ni sawa na kuumiza moyo wako pasipo na sababu za msingi.

Huwa nikimtazama Daniel Sturridge kwa sasa, naukumbuka wimbo Ngololo kutoka kwa msanii Diamond Platinumz.Nadhani wakati Diamond anafanya video ya wimbo huu angemchukua na Sturridge amsaidie kwenye kucheza,jamaa anavipaji vingi sana. Sturridge amecheza mechi 25 tu msimu huu lakini ameshafunga mabao 20 na kutengeneza mengine 7. Kuna mtu anakuambia kuwa Sturridge na Suarez ni wachoyo, wabinafsi, hivi unatumia kigezo gani?. Wote kwa pamoja wametengenezeana na kuwatengenezea wenzao mabao 18, ulitaka wafanye nini zaidi?

Kuna muda hauhitaji kuwa na wanajeshi milioni 2 ndipo uamue kwenda vitani, unaweza ukawa na wanajeshi wachache tu kama vijana wa Brendan Rodgers na mambo yakafana. Kila siku anapochagua kikosi cha kwanza hakuna mchezaji wa akiba ambaye kama timu inazidiwa ana uwezo wa kuja kubadilisha matokeo. Unajua kwa nini Liverpool haihitaji msaada wa mchezaji ambaye yuko benchi? jibu ni rahisi tu, Liverpool wanakuchakaza mapema tu mpaka wanapomwingiza Iago Aspass, siku nyingi ulishatolewa manundu. Arsenal ndani ya dakika 18, alikuta alishachezea bao 4-0. Unadhani hata Brendan angeniingiza mimi mngenijua? mngejali? hapana, ningeweza pengine kupiga Hat-trick. Ukiwa na wanaojua, na wewe unaujua tu.

Liverpool nadhani walishatimiza lengo lao la msingi la kuhakikisha wanamaliza kwenye moja ya nafasi nne za juu ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Ulaya ambayo wameikosa kwa muda mrefu lakini,kama watapata ubingwa wa EPL,itakuwa ni kama zawadi tu kwa kaka mkubwa Steven Gerrard ambaye pamoja na mataji lukuki,pamoja na uwezo wake wa hali ya juu,hajawahi kushinda taji la ligi kuu huku,mtu kama Tom Clevery wa Man United akishinda medali hiyo.Hivi hapa soka limetenda haki kweli?

Bado ni mapema kusema kuwa Liverpool watakuwa mabingwa wa EPL msimu huu kwa sababu ya mechi ngumu ambazo wamebakiza,hasa zile zinazowahusisha timu za Chelsea na Man City ambao nao wanawania ubingwa lakini,hakuna kinachoshindikana kwenye mchezo wa soka.Goli linafungwa kwa sekunde moja,kila la kheri Rodgers na wanao na kama vipi,endeleeni tu kula ujana muda ndiyo huu.


Kwa leo,naishia hapa.Kama unachochote na ungependa kushirikiana na mimi unaweza kunitafuta kwenye ukurasa wangu wa Facebook kwa jina la Oscar Oscar Jr au kuchati na mimi kupitia whatsapp kwa namba +255789784858

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!