Searching...
Image and video hosting by TinyPic
23 April 2014
Wednesday, April 23, 2014

NIONAVYO MIMI:KUNA MUDA SOKA LA KARNE YA 19 LINA MAANA.

Na Oscar Oscar Jr
+25578978485


Jose Mourinho ni moja kati ya makocha bora Duniani kwa sasa uwe unapenda au hupendi.Ameshinda mataji mawili ya ligi ya mabingwa Ulaya akiwa na klabu mbili tofauti (Inter Millan na Fc Porto),umetwaa ubingwa wa ligi kuu kwenye nchi nne tofauti(Uingereza,Hispania,Italia na Ureno) na wakati wewe ukisonya kwa mbinu zake zinazokuboa,mwenzio jana alikuwa anavunja rekodi ya Sir Alex Ferguson ya kucheza nusu fainali ya UCL mara saba,Mourinho jana kacheza kwa mara ya nane.Upo hapo?

Unaweza kuwa hakupendezwa na namna mbinu za Mourinho zilivyo haribu burudani ya mchezo wa soka mbele ya Atletico Madrid ambao wako kwenye ubora wa hali ya juu msimu huu lakini ukweli utabaki pale pale,huu mpira wa kuzuia ndiyo uliyomuweka Mourinho mjini.Tuache Uongo,ni lini Mourinho amewahi kucheza mpira wa burudani? wakati wewe ukiendelea kusonya,mwenzio anakaribia rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu huku akiwa na klabu tatu tofauti!

Akiwa na klabu ya Inter Millan msimu wa 2009/2010 alikutana na Barcelona kwenye hatua kama hii na akafanikiwa kushinda 3-1 kule San siro.Alipotua Camp Nou,alifungwa bao 1-0 ingawa alifanikiwa kwenda fainali na kutwaa Ubingwa.Sioni tofauti kati ya  mchezo ule na alichokifanya mbele ya Atletico Madrid.Hakuna mtu ambaye angemsifia kwa kucheza soka safi endapo angepoteza mchezo lakini,alisifika kwa kutwaa taji hilo kwa mara ya pili tena  akiwa na klabu ya pili tofauti.

Unapocheza na timu kama Atletico Madrid tena Ugenini mbele ya watu kama Koke na Gambi Hernandez kwenye sehemu ya kiungo huku Diego Costa mwenye mabao 27 ya La Liga msimu huu akiongoza safu ya ushambuliaji,hauhitaji kuwa na mbwembwe.Real Madrid walichezea kichapo kwenye La Liga kwao Bernabeu huku Barcelona wakisambaratishwa kwenye robo fainali ya UCL,kwa nini usicheze soka la karne ya 19 ili ubaki salama?

Koke ndiye mchezaji anayeongoza kwenye ligi ya Hispania kwa kupiga pasi nyingi za mwisho,mpaka sasa ameshatengeneza mabao 13.Ni lazima umtengenezee mazingira maalumu ya kuzuia pasi zake na ndiyo maana walinzi Gary Cahil na John Terry waliwekewa tena mlinzi mwingine ambaye ni Mikel Obi.Ramires kazi yake ilikuwa ni kumkaba mbrazil mwenzie Fillipe Luiz ambaye alicheza beki ya kushoto huku Willian naye akipambana na beki wa kulia Juan Francisco.Unamjua Mourinho au Unamsikia?

Atletico Madrid ambao walimiliki mpira kwa asilimia 69 na kupiga mashutu 25,walifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini hawakufanya hilo.Atletico walitakiwa kupata goli ili kuikaribisha "Plan B" ya Mourinho ambaye kwa vyovyote vile ni lazima angefunguka kusaka goli la ugenini na hapo ndipo huenda angeangamizwa.Mechi yake na PSG kule Ufaransa alitaka pia kuzuia lakini baada ya kufungwa,akajiachia.Atletico jana waligoma kufunga na Mourinho akagoma kufunguka,kwani kuna tatizo?

Matokeo ya suluhu pacha bado yanaufanya mchezo wa marudiano kuwa mgumu kwa pande zote mbili.Chelsea watakuwa na faida ya kucheza mbele ya mchezaji wao namba 12 (Mashabiki) huku watoto wa Diego Semeon wakihitaji sare yoyote ya magoli kuwapeleka fainali ya michuano hiyo.

Mikel Obi na Frank Lampard wataukosa mchezo wa marudiano kutokana na kupewa kadi mbili za manjano lakini sidhani kama ni tatizo kwa sababu Mourinho atamrejesha Hazard na Oscar kwa ajili ya kuongeza kasi ya mchezo na kutafuta bao kwa njia ya mashambulizi ya kushitukiza ambapo Chelsea wamekuwa wakifanya vizuri chini ya Mourinho.Sitegemei tena kuona soka la karne ya 19 pale darajani labda kama Chelsea wanaweza kupata magoli ya mapema,jambo hilo linaweza kujirudia.

Mourinho kwa miaka mitatu mfululizo amekuwa akitolewa katika hatua hii ya nusu fainali ya mabingwa Ulaya.Msimu wa 2010/2011 alitolewa na Barcelona ambao walienda kutwaa taji hilo,2011/2012 alitolewa na Bayern Munich ambao walienda kupoteza fainali mikononi mwa Chelsea ya Roberto Dimateo na 2012/2013 ,alipoteza mbele ya Borussia Dortmund ambao walienda kupoteza fainali mbele ya Bayern Munich.Rekodi yake si nzuri ya hivi karibu na asingependa jinamizi hili liendelee kumtafuna.

Soka la karne ya 19 kuna muda naona linalipa,West Ham United walipotua Stanfford Bridge msimu huu,walicheza soka la kupaki Bus na wakafanikiwa kuondoka na alama moja baada ya kupata sare,timu kama Arsenal na Manchester City ambao walifika darajani na kujiachia,walijikuta wote wakichezea kichapo.Pamoja na kuwa Mourinho alilalamikia mchezo huo lakini,yeye ndiye bingwa na jana ndicho kilichomponyesha.Unadhani soka la 19 halikuwa na faida kwa timu ya Chelsea? hapana,bora nusu shari kuliko shari kamili.

Ac Millan ya kaka,Balotelli na wenzao,walipotua Vicente Calderon walijikuta wakichezea kichapo.Xaiv Hernandez,Lionel Messi na wenzao,nao walichezea kichapo.Ulitaka Mourinho afanye nini? kuna uwezekano mkubwa kuwa hakutimiza matakwa yako lakini nadhani binafsi alipata zaidi ya asilimia 80 ya malengo yake.Raha jipe mwenyewe! Bado mechi iko wazi kwa yeyote kati yao kuweza kusonga mbele,tukunatane darajani siku ya jumatano.

Naomba kuishia hapa,kama unalolote na ungependa kuchati na mimi,unaweza kunitafuta kwenye ukurasa wangu wa facebook au kuchart na mimi kwa whatsapp kwa namba +255789784858.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!