Searching...
Image and video hosting by TinyPic
19 March 2014
Wednesday, March 19, 2014

NIONAVYO MIMI:SOKA LETU LINAHITAJI PIA FACEBOOK.

Na Oscar Oscar Jr
0789-784858

Mwezi Agosti mwaka 2012 serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,iliendesha zoezi la sensa ya watu na makazi nchini nzima na mwezi desemba mwaka huo,Rais Jakaya Mrisho kikwete akiwa viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam alitangaza matokeo ya sensa hiyo ambapo Tanzania ina watu zaidi ya Milioni 44 na katika idadi hiyo,watu wenye umri kati ya miaka 18-35 ndiyo wako wengi.

Siku hizi ukikutana na watu 10 wenye umri kati ya miaka 18-35,kuna uwezekano mkubwa sana watu 7 kati yao wakawa wanatumia moja kati ya mitandao ya kijamii kama Facebook,Twitter,Instagram,Youtube,whatssup au yote.Hii yote imechangiwa na maendeleo ya tekinolojia ya habari na mawasiliano duniani kote.

Mwandishi wa habari za soka wa Al-Jazeera anayeripoti habari za soka Uk na Ulaya,Lee Wellings mapema mwaka huu alisema "Huu ni mwaka wa kombe la Dunia kwenye Twitter" katika makala hiyo amesema sio kwamba hii ni mara ya kwanza kwa kombe la Dunia kufanyika huku mtandao wa Twitter ukiwepo bali,ni mwaka ambao Twitter imekuwa maarufu na kupata watumiaji wengi kuliko miaka yote ya nyuma.

Hapa kwetu timu nyingi za soka hasa zinazopatikana nje ya jiji la Dar es salaam zimekuwa na tabia ya kulalamika kuwa hazipewi sana nafasi kwenye vyombo vya habari kama Magazeti na Redio.Kuna uwezekano madai yao yakawa na ukweli na sababu kubwa inaweza kuwa ya kibiashara,watu wanapenda kusikia habari zaidi za Simba,Azam na Yanga na tofauti na hapo,Gazeti haliuzi.

Tabia ya vyombo vya habari kuripoti habari za timu kubwa kila siku sio Tanzania tu,hata huko kwa wenzetu mambo ndivyo yalivyo.Ukichunguza Hispania kila siku utakutana na habari za Barcelona,Real Madrid na Atletico Madrid kwa kipindi hiki na ni vigumu kukuta klabu ya Celta Virgo au Almeria kuteka vyomba vya habari labda kuwe na tukio lisilo la kawaida.Ukiangalia Ujerumani utakutana na habari za Bayern Munich,Borrusia Dortmund ndiyo zimepamba vichwa vya habari,Italia ni Juventus,Napoli na timu nyingine kubwa,habari ndiyo hiyo.

Tofauti na sisi,Ulaya hata timu ndogo utakuta inamiliki vyombo vyake vya habari kama magazeti na Luninga hivyo wanakuwa huru kutoa taarifa kwa mashabiki wao muda wowote.Hapa kwetu ukiondoa timu ya Azam inayomiliki Tv,wengine hamna kitu na hata wachache wenye magazeti kiukweli,hayana mvuto.Wenzetu wamestuka mapema na kwa sasa karibu kila timu ina akaunti ya Facebook,Twitter,Instagram,Youtube n.k

Kuna baadhi ya klabu hapa nyumbani kama Azam,Coastal Union,Yanga,Mtibwa Sugar wameshaanza kutumia mitandao hii ya kijamii lakini,nadhani wanakosa ubunifu na ndiyo maana wanawafuasi wachache.Arsenal kwenye akaunti yao ya Twitter wameweka utaratibu wa kumualika mchezaji mmoja mmoja na kuwapa fursa mashabiki wa timu hiyo kufahamu mengi kupitia wachezaji na viongozi wa timu hiyo.Wana kipindi cha maswali na majibu kwenye akaunti yao,sio vibaya kama tunaweza kuiga hili.

Mashabiki na wapenzi wa timu zetu,wanakiu ya kuwafahamu kiundani wachezaji wao,kwa kutegemea tu magazeti na Redio zinazomilikiwa na watu wengine sio rahisi kufikia malengo.Hakuna Redio nchini inayojadili mchezo wa soka kwa zaidi ya dakika 60 kwa siku,ila muziki hadi vipindi vya dakika 240 vipo.Vilabu ni lazima vitafute njia mbadala ya kujitangaza na binafsi naona mitandao ya kijamii inaweza kusaidia sana.

Tatizo la viongozi wetu ni kutaka kufanya kila kitu wao hata kwenye maswala yanayohitaji taaluma wasizokuwa nazo.Ndiyo maana huwa sishangai hata leo hii nikiingia mtandaoni na kukuta "Profile" ya Juma Jabu bado ikionyesha ni mchezaji wa Simba sc.Kwa namna ajira ilivyokuwa ngumu kwa sasa nchini,unauwezo wa kumuajiri kijana aliyemaliza chuo kikuu na mwenye ujuzi wa taaluma ya tekinolojia ya habari na mawasiliano na ukamlipa pesa isiyozidi 700,000 tu kwa mwezi na akakufanyia kazi yenye ubora.

Leo hii klabu ya Yanga ikitangaza kuwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi atakuwa LIVE kwenye akaunti yao ya Twitter na atakuwa akijibu maswali ya mashabiki wa timu hiyo kuanzia saa 4-5 usiku,kuna uwezekano siku hiyo watu wasilale.Leo hii ukisikia Mwenyekiti wa Simba atazungumza na wanachama na mashabiki wa simba kwenye mtandao,hata kama watasema itakuwa ni saa 9 usiku,watu watamsubiri tu.

Ukitembelea tovuti ya FC Barcelona utakuta inapatikana kwenye lugha 7 tofauti,lengo hapa ni kuweza kuwafikia mashabiki wao wengi popote walipo duniani.Wakati timu kama Barcelona ikiendelea kusogea karibu na mashabiki wake kwa njia ya mtandao,klabu za Rinho Rangers,Mgambo shooting,Kagera sugar na nyingine nyingi,zinasubiri Kutangazwa na magazeti na Redio za Dar es salaam!!

Maisha yamebadilika na dunia imeendelea kuwa kijiji,kuna watu kutokana na majukumu yao hawapati kabisa muda wa kusoma magazeti wala kusikiliza Redio iwe kazini au maofisini.Ukiweka habari za timu yako mtandaoni,muda wote zitakuwepo na mtu atakuwa na nafasi ya kusoma,kuona au kusikilizaa muda wowote.Kipindi cha Redio kikikupita au cha Luninga,ndiyo basi tena.Hata hizo Redio na Magazeti siku hizi zinalazimika kupatikana pia mtandaoni,nyie JKT Oljoro na Tanzania Prisons hamjastukia tu?

Klabu kupitia mitandao ya kijamii inauwezo wa kuwavuta mashabiki wao karibu hata kwa kuwapa jukumu la kumchagua mchezaji bora wa mwezi au wa kila mchezo kupitia mitandao hiyo.Pia mnaweza kutengeneza pesa kwa kuanzisha namba maalumu ya kutuma ujumbe wa kumchagua mcheza bora wa mwezi wa timu na mashabiki wanaweza kutozwa hata shilingi 500 tu kwa ujumbe mmoja.Kwa utitiri wa mashabiki wenu,mtaingiza shilingi ngapi kwa mwezi?

Swala la mtandao sio kwa timu za ligi kuu tu,hata Pamba,Lipuli,Tesseme,Polis Tabora,JKT Kanembwa nao wanaweza kutumia fursa hii na kuweza kuwatangaza wachezaji wao.Wekeni picha zao za video kwenye You tube dunia nzima itaona na mnaweza kuwauza wachezaji wenu kwa bei safi kabisa sehemu yoyote Duniani.Hata kama unakipaji namna gani kama hutoki nje na kukionyesha,hakuna atakaye kuona. siku njema.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!