Searching...
Image and video hosting by TinyPic
20 March 2014
Thursday, March 20, 2014

HATIMAYE MOYES KAANZA MAJIGAMBO.



 Meneja wa Manchester United anayekabiliwa na shinikizo David Moyes amesisitiza kwamba hana presha baada ya timu yake kufanya mapinduzi makuu dhidi ya mabingwa wa Ugiriki Olympiakos na kufika robofainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. 

Moyes alishuhudia ushindi adimu sana Old Trafford Jumatano usiku United walipolipa deni la mabao 2-0 kutoka mechi ya awamu ya kwanza ya 16 bora kwa ushindi wa 3-0 uliotokana na mabao matatu ya Robin van Persie. 

Huku United wakiwa alama 18 nyuma ya viongozi ligi, na 12 kutoka eneo la nne bora baada ya kulazwa na Liverpool 3-0 Jumapili, kazi ya meneja huyo wa zamani wa Everton ilikuwa hatarini.
Vyombo vya habari vya Uingereza vilikuwa vimedokeza kwamba hatima yake ingekuwa hatarini licha ya matokeo ya mechi hiyo ya Olympiakos, lakini alisema ana imani kwamba anaungwa mkono kikamilifu na waajiri wake. 

“Sina presha yoyote kutoka kwa klabu,” aliambia wanahabari.
“Inatoka kwenu. Tunajua ile kazi tunayofaa kufanya. Ni kubwa labda kushinda nilivyodhania nilipotua hapa mara ya kwanza.
“Kuna hizi stori za mchezaji huyu kukosana na timu, au mwingine, lakini huo ni upuuzi. Watu wanatafuta sababu za kueleza ni kwa nini hatufanikiwi, lakini ni kwa sababu hatuchezi vyema.”
United hawajawahi kupindua kichapo cha mabao mawili katika awamu ya muondoano Ligi ya Mabingwa, lakini Moyes hakuwa tayari kueleza ufanisi wao kama kipindi kikuu cha kuamua mambo.

“Watu labda watadhani huu ni wakati utakaoathiri kazi na taaluma za watu, lakini siitazami hivyo kwa sababu klabu haioni hivyo,” akasema raia huyo wa Scotland ambaye alitia saini mkataba wa miaka sita mwaka jana.
“Ninaona nikiwa hapa muda mrefu. Ninafikiri tuna kazi nyingi sana ya kufanya, lakini hayo ni matokeo mazuri na tunataka kusalia katika dimba hili.” 

Van Persie alianza ufungaji mabao kwa kufunga penalti dakika ya 25 baada ya kuangushwa na Jose Holebas na kisha akakomboa mabao yote kwa bao dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kwa kufunga kutoka kwa krosi ya chini ya Wayne Rooney. 

Straika huyo wa Uholanzi aliwahakikishia ushindi kwa frikiki dakika saba baada ya kipindi cha pili kuanza, lakini United walilazimika kuvumilia mashambulio makali na wanafaa kushukuru kipa David de Gea aliyewaokoa.
Van Persie aliondolewa kwa machela dakika za mwisho za mechi baada ya kujeruhiwa goti, lakini Moyes alisema jeraha hilo “si baya sana”.

Pia alimsifu sana kiungo wa kati mkongwe Ryan Giggs, ambaye licha ya umri wake wa miaka 40, alitamba sana kwa kutoa pasi safi, kuzipokea na kusaidia kuunga mabao mawili ya kwanza.
“Inashangaza, zile mechi amecheza katika Ligi ya Mabingwa,” Moyes alisema.
“Alikuwa mzuri sana – zile pasi alizotoa na kusaidia ufungaji wa mabao hayo mawili, uchezaji wake kwa jumla wa soka. Ni wa kipekee.” 

United watajua timu watakayokabiliana nayo robofainali Ijumaa, na ingawa masaibu yao kwenye Ligi ya Premia yanawafanya wakose kupigiwa upatu kushinda, Moyes anaamini wanaweza kufanya hivyo.
“Huenda sasa tutaenda kwenye awamu hiyo tukiwa hatupigiwi upatu,” akasema.
“Tunatumai tunaweza kufanya hivyo. Sioni sababu ya kutufanya tushindwe.
“Ninafikiri klabu hii inaweza. Tukicheza kadiri ya uwezo wetu, jambo ambalo hatujafanya sana, ninafikiri tunaweza kukabili timu yoyote ile.”

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!