Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 February 2015
Monday, February 02, 2015

Makala: Atsu na Bony kidogo wamefunika aibu ya “masupastaa”




Na Chikoti Cico



Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) linakaribia kufikia ukingoni nchini Guinea ya Ikweta kwa timu nne kuingia kwenye hatua ya nusu fainali ambapo Ivory Coast itacheza dhidi ya Jamhuri ya Watu wa Congo na Ghana dhidi ya Wenyeji Guinea ya Ikweta katika kutafuta timu mbili zitakazoingia fainali ya michuano hiyo.

Inawezekana ni michuano ambayo haikuwasisimua mashabiki wa soka barani Afrika hasa kutokana na wachezaji wengi ambao wanacheza ligi kubwa duniani kushindwa kuonyesha viwango vyao ambavyo vimezoeleka kuonekana kwenye ligi mbalimbali kama ya Uingereza, Bundesliga, Seria A na League 1.

Yaya Toure mshindi za tuzo ya mwanasoka bora Afrika anayekipiga kwenye klabu ya Manchester City hakuonyesha kiwango kilichotegemewa na wengi.

Gervinho anayekipiga AS Roma ya nchini Italia anakumbukwa zaidi kwa kumpiga kofi mchezaji wa Guinea Naby Keita wakati timu hizo zilipokutana kuliko ubora wake wa kukokota mpira anapoichezea klabu yake ya Roma.

Mshambuliaji wa klabu ya Borrusia Dortmund na nahodha wa timu ya taifa ya Gabon Pierre-Emerick Aubameyang mpaka timu yake ya taifa inatolewa kwenye hatua ya makundi alikuwa amefunga goli moja tu dhidi ya Burkina Faso na hakuonyesha ule ubora wake uliotegemewa na wengi.

Mshambuliaji wa klabu ya Newcastle United na timu ya taifa ya Senegal Papiss Cisse pamoja na kutokuanza kwenye mechi nyingi za hatua ya makundi lakini pia bado hakuonekana kama ni moja ya mshambuliaji hatari anayekipiga kwenye ligi ya Uingereza.

Inawezekana wachezaji hawa “masupastaa” ambao timu zao za taifa zilikuwa na matagemeo makubwa kwao wanaweza kujitetea kwamba wasingeweza kuzibeba timu zao wao wenyewe lakini ukweli utabaki pale pale kwamba wengi wameshindwa kuzing’arisha timu zao za taifa na kiujumla wameshindwa kuing’arisha michuano hii ya AFCON kwa mwaka 2015.

Lakini kwenye hatua ya robo fainali wachezaji wawili wanaocheza ligi kuu nchini Uingereza Christian Atsu na Wilfried Bony walituonyesha nini ambacho wachezaji “masupastaa” walitakiwa kukifanya toka mwanzo wa michuano hii mikubwa Afrika, walituonyesha kile ambacho mashabiki wa soka la Afrika walitakiwa kukiona na kujivunia kwamba hakika tuna vipaji mahiri kwenye bara hili lenye nchi zaidi ya 54.

Magoli mawili yaliyofungwa na Wilifried Bony kwenye mchezo dhidi ya Algeria yalitosha kuihakikishia timu ya taifa ya Ivory Coast kuingia kwenye hatua ya nusu fainali lakini nyuma ya magoli hayo Bony alituonyesha kwanini mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Uingereza timu ya Manchester City ilimnunua mchezaji huyo kutoka Swansea kwa ada ya pauni milioni 25.

Lakini pia pamoja na kwamba ni magoli pekee kwa mshambuliaji huyo toka kuanza kwa michuano hii ya AFCON lakini yalikuwa ni magoli ambayo yaliyoonyesha tofauti ya mchezaji anayecheza pale Asec Mimosas nchini Ivory Coast na anayekipiga klabu ya Manchester City ya nchini Uingereza.

Tofauti ambayo haikuonekana toka mwanzoni mwa michuano hii ambapo karibu wachezaji wote walionekana wako sawa tu. Unaweza kusema Bony ameifunika aibu ya “masupastaa” wa Afrika ambao walishindwa kutimiza matarajio ya wengi.

Mchezaji mwingine aliyeinogesha AFCON na kuifunika aibu ya “masupastaa” wa Afrika kwenye michuano hiyo ni Christian Atsu anayeichezea klabu ya Everton kwa mkopo akitokea klabu ya Chelsea, magoli mawili ya Atsu dhidi ya Guinea yaliiwezesha Ghana kuingia hatua ya nusu fainali huku moja ya magoli hayo akifunga kwa shuti kali toka umbali wa yadi 25.

Huyu ni mchezaji mwingine anayekipiga kwenye ligi kuu nchini Uingereza na magoli kama haya ndiyo yaliyokuwa yanasubiriwa na mashabiki wengi wa soka barani Afrika unaweza kusema kwa kiasi flani ametimiza matarajio ya mashabiki wa timu ya taifa ya Ghana na Afrika kwa ujumla.

Mwisho nimalizie kwa kuzitakia kila la kheri timu za Ghana, Ivory Coast, Guinea ya Ikweta na Jamhuri ya watu wa Congo kwenye hatua ya nusu fainali nikiamini wachezaji wa timu hizo watatupa burudani lakini pia kutuacha na kumbukumbu nzuri ya michuano ya AFCON kwa mwaka 2015.

“They call it Africa, we call it home” (Wanapaita Afrika, tunapaita nyumbani)
NAWASILISHA

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!