Searching...
Image and video hosting by TinyPic
19 October 2014
Sunday, October 19, 2014

Uchambuzi; Ndanda fc wanapaswa kuwa waoga.


Na Oscar Oscar Jr

Timu ya Ndanda jana wamejikuta wakipoteza mchezo wao wa tatu mfululizo mbele ya timu ya Ruvu Shooting kutoka mkoa wa Pwani kwa kuchapwa mabao 3-0. 

Ndanda walianza ligi kuu kwa ushindi wa bao 4-1 dhidi ya wageni wenzao kwenye ligi timu ya Stand United kabla ya kuja kufungwa na Mtibwa Sugar na baadaye, Coastal Union.

Kwa nini Ndanda wanafungwa? Tangu walipopanda daraja, Ndanda  wamekuwa ni timu inayoungwa mkono sana na wakazi wa mikoa ya Kusini. 

Ushindi wao wa mchezo wa kwanza, uliwafanya waone tayari wanaweza kupambana kitu ambacho kikawafanya wajiamini kupita kiasi. Ndanda walisahau kuwa ushindi wao, ulikuwa kama tangazo la vita kwa timu nyingine za ligi kuu.

Kwenye soka kuna baadhi ya mambo yanatokea bila kupangwa. Unapoona timu inashinda bao 8-0 kama walivyofanya Southampton jana mbela ya Sunderland, sio kwamba walipanga. 

Unavyoona Mbeya City akimaliza kwenye nafasi ya tatu msimu uliopita, sio kwamba walipanga. Kuna mambo yanatokea kama Surprise na naamini, nafasi ya tatu kwa mbeya City ilitokea kama Surprise kwao.

Ndanda wao hawataki surprise, wamepanga kabisa kumaliza nafasi ya tatu kama walivyofanya Mbeya City msimu uliopita. Hii hali imeongeza presha kwa wachezaji na benchi lao la ufundi kitu kinachopelekea wachezaji wao kucheza huku wakiwa na mzigo mzito kichwani wa kumaliza kwenye nafasi ya tatu!

Ndanda wanapaswa kuwa waoga kama walivyo Mbeya City. Nilibahatika kushuhudia michezo zaidi ya 10 msimu uliopita ya Mbeya City wakiwa nyumbani. 

Siku zote walitafuta goli kwa machale huku muda wote, wakifanya kazi ya kuzuia kama timu na ndiyo maana, michezo yao minne ya kwanza nyumbani, walishinda mmoja tu. 

Kuwa na mashabiki wengi sio kigezo cha kupanga malengo ya juu kuliko uwezo wa timu. Ndanda wao kila kukicha, wanawaza kupata matokeo kama ya  Mbeya City ya msimu uliopita kwa sababu tu wanamashabiki wanaosafiri nao kila mahali! 

Ndanda wanapaswa kuwa na malengo ya kutoshuka daraja msimu huu ili waendelee kupata uzoefu wa ligi kuu na ikitokea kumaliza kwenye nafasi za juu, basi iwe kama surprise kwao na bonus.

Timu ya Azam ilihitaji ubingwa wa ligi kuu bara kwa muda mrefu sana lakini, hawakuwa na haraka walilazimika kupata uzoefu wa ligi kwanza na baadaye, mambo yalianza kukaa sawa. 

Unapokuwa na malengo makubwa, presha inakuwa kubwa sana kwa wachezaji na wanapofungwa mchezo, wanahisi kama hawakustahili kupoteza. 

Mchezo wao wa kwanza nyumbani, walipaswa kuiheshimu Ruvu Shooting kama timu kubwa kwao licha ya kuwa haikuwa imeshinda mchezo hata mmoja kabla ya mechi ya jana. 

Walitakiwa kutambua kwamba, Ruvu Shooting walikuwa wanahitaji alama tatu kwao ili nao wajiweke pazuri. Ndanda wangezui zaidi na kutumia nafasi chache walizotengeneza kujipatia bao.

Hata kama wangepata sare, naamini mashabiki wa Ndanda, wangeridhika tu. Mbeya City msimu uliopita walianza kwa sare tasa dhidi ya Kagera Sugar nyumbani na mashabiki waliridhika. 

Unapotaka mafanikio ya Mbeya City, unapaswa kuiga na uoga wao.


0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!