Searching...
Image and video hosting by TinyPic
31 October 2014
Friday, October 31, 2014

Uchambuzi: Manchester City vs Manchester United


Na Chikoti Cico

Katika mfululizo wa mechi za ligi kuu ya Uingereza moja ya mechi inayosubiriwa kwa hamu na wapenzi wengi wa soka, ni mchezo unaowakutanisha Manchester City dhidi ya Manchester United maarufu kama “Manchester Derby”.

Mchezo utakaopigwa siku ya Jumapili saa 10:30 kwa saa za Afrika Mashariki kwenye dimba la Etihad.

Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini anaingia kwenye mchezo huo huku akiwa na mwenendo mbaya wa matokeo baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo. Alipoteza mmoja wa ligi kuu  dhidi ya West Ham United na mwingine, kwenye Capita One Cup dhidi ya Newcastle United.

Wakati huo huo timu ya Manchester City inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 17 kati ya michezo tisa, itawakosa viungo David Silva aliyeumia goti kwenye mchezo dhidi ya Newcastle huku akitarajiwa kukaa nje kwa wiki tatu ama nne pia, itamkosa Frank Lampard ambaye bado ni majeruhi.

Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa washambuliaji wa Manchester City, Edin Dzeko na Sergio Aguero wote wamefunga magoli manne katika mechi tano za ligi dhidi ya Manchester United huku pia, kiungo Yaya Toure akifunga magoli matatu kati ya mechi tatu zilizopita za ligi alizocheza dhidi ya Manchester United.

Wakati huo huo, takwimu zinaonyesha kati ya mechi sita zilizopita za ligi Manchester  City wameshinda michezo mitano na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya United.

Kikosi cha Manchester City kinaweza kuwa hivi: Hart; Zabaleta, Kompany, Mangala, Clichy; Toure, Fernando, Navas, Milner; Aguero, Dzeko.

Kocha wa timu ya Manchester United mdachi Luis Van Gaal anatarajia kuwakosa mshambuliaji Radamel Falcao, kiungo Jesse Lingard na mabeki Phil Jones, Jonny Evans na Paddy McNair ambao ni majeruhi.

Kiungo na nahodha wa United, Wayne Rooney ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kutokucheza mechi tatu anatarajiwa kucheza kwenye mtanange huo huku pia Valencia nae akitarajiwa kurejea uwanjani baada ya kuwa nje kwasababu ya majeruhi.

Takwimu zinaonyesha kuwa nahodha wa Manchester United, Wayne Rooney anaongoza kwa kufunga magoli kwenye “Manchester derby” huku akifunga magoli 11 kwenye mashindano yote yaliyozikutanisha timu hizi mbili huku magoli manane kati ya hayo 11, akiyafunga kwenye ligi.

Rooney amefunga magoli manne katika mechi tano zilizopita za ligi dhidi ya City zilizochezwa Etihad.

Kikosi cha Manchester United kinaweza kuwa hivi: De Gea; Rafael, Smalling, Rojo, Shaw; Blind, Fellaini; Herrera, Di Maria; Rooney; Van Persie

Rekodi zinaonyesha kati ya mechi 150 za Manchester Derby, Manchester City ameshinda mara 42 huku Manchester United ikishinda mara 59 na wametoka sare mara 49.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!