Searching...
Image and video hosting by TinyPic
10 August 2014
Sunday, August 10, 2014

Ligi ya Seria A inaelekea ICU


 
Na CHICOTI jr (Cico cicod)
  0755 700076

Ni kipindi cha usajili kila timu inajaribu kupata sahihi ya mchezaji bora na mwenye kuleta manufaa kwenye timu, unapata habari Toni Kroos (24) amesajiliwa na Real Madrid, upande wa pili unasikia Barcelona imemsajili Luis Suarez (27), ukirejea Uingereza unaambiwa Chelsea imemsajili Diego Costa (25) na Arsenal ikimsajili Alexis Sanchez (25), kule Ujerumani Bayern Munich imemsajili Lewandoski (25) na PSG imemsajili David Luiz (27).

Unapoenda Italia unaambiwa Juventus imemsajili Patrick Evra (33), AS Roma ikimsajili Ashley Cole (33) na Inter Milan ikimsajili Nemanja Vidic (32) na hapo ndipo wasiwasi dhidi ya ligi kuu ya Italia unapoingia kichwani. 

Nini kimetokea nchini Italia mpaka ligi yao kuanza kusajili wachezaji wenye umri wa kula pensheni, wachezaji ambao washatumika vya kutosha pale Uingereza mpaka jasho lao la mwisho kudondoka . 

Evra, Cole na Vidic wote wataonekana kwenye ligi ya SERIA A msimu wa 2014/2015, hapa ndipo ubora wa ligi ya Italia unaponitia shaka na haishangazi sana unaposikia Franscesco Totti (37) anapomfananisha Gervinho na Christiano Ronaldo. 

Takwimu zinatuambia 2010/2011 ndiyo mara ya mwisho kwa timu kutoka Italia kufika hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya “UEFA CHAMPIONS LEAGUE” , hii inaonyesha jinsi gani ligi ya Italia imepoteza mwelekeo na kukosa ushindani wa kuifanya iwe bora tena. 

Unajiuliza utawala wa AC Milan umekwenda wapi, ubora wa Inter Milan umekwenda wapi na umahiri wa Juventus umefia wapi. 

Skendo ya mwaka 2006 ya upangaji matokeo (Kiitaliano, Calciopoli) ambayo ilihusisha timu za Juventus, AC Milan, Fiorentina ,Reggina na Lazio na kupelekea kuadhibiwa na shirikisho la soka nchini Italia, ilichangia kwa kiasi kikubwa kuchafua umaarufu wa ligi ya Italia, na kukosa mvuto mbele ya mashabiki wa soka duniani. 

Zaidi ya kupoteza mvuto mbele ya mashabiki wa soka hata wachezaji bora duniani wameikimbia ligi hiyo, orodha ni ndefu ya wachezaji mahiri walioamua kuondoka Italia hii yote inaonyesha jinsi gani timu kama AC Milan, Inter Milan, Juventus, Lazio, Napoli zimekosa mvuto mbele ya wachezaji mahiri duniani. 

Baadhi ya wachezaji mahiri walioamua kufungasha virago ni Kaka, Ibrahimovic, Thiago Silva, Cavani, Lavezzi, Pastore, Verrati na hata kocha Carlo Ancelotti alitimka. 

Kutoka kwenye vijiwe vya kahawa mpaka kumbi za starehe wapenzi wa soka duniani wanaziongelea ligi za nchi nyingine na sio Italia tena.

Ligi ya Italia inaongelewa kwa uchache sana kwasababu ya kupoteza mvuto hata mechi kubwa ya wapinzani wa jadi maarufu kama “Milan Derby” kati ya AC Milan dhidi ya Inter Milan imepoteza mvuto wa kuangalia. 

Inawezekana ligi kuu ya Italia SERIA A inapitia kipindi kigumu hivyo tusubiri labda muda utatuambia, yawezekana makali, ubora na umahiri wake utarejea tena kwa miaka mingi ijayo ila kwasasa tuwaache kina ASHELY COLE, NEMANJA VIDIC NA PATRICK EVRA wakale pensheni yao kwenye miji ya Milan, Roma, Napoli ama Siena. 

NAWASILISHA @CHICOTI jr (Cico cicod) 0755 700076

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!