Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 August 2014
Saturday, August 02, 2014

ANGALAU AKINA BOBAN WALITHUBUTU.



Na Oscar Oscar Jr
+255789784858

Watanzania wengi hatuna moyo wa uthubutu na uvumilivu na hata wachezaji wetu waliowahi kwenda nje, wapo waliokosa uvumilivu na hatimaye wakarudi mapema. Nizar Khalfan, Henry Joseph na hata Haruna Moshi maarufu kama "Boban" naye yumo kwenye orodha hiyo lakini, angalau wao waliweza hata kuthubutu.

Tuna wasomi wengi sana hapa nchini tena wa kutoka vyuo vikuu na wapo mtaani tu. Ukimwambia kuna nafasi za kazi nchini Malawi, hana uthubutu wa kwenda. Ukimwambia kuna upungufu wa waalimu kule Zimbabwe, hata siku moja hawezi kuomba kazi hiyo. Lakini kwenye vijiwe vya kahawa na vibanda umiza ndiye wa kwanza kupendekeza wachezaji wetu waende kucheza soka nje ya nchi!

Wachezaji wetu bado ni wale wale wa juzi, jana na leo. Wanaelimu ya kawaida kabisa, hata uwezo wao wa kuchanganua mambo madogo madogo tu ni ule ule wa juzi, jana na leo lakini, angalau wameweza kuthubutu kwenda nje na baada ya kushindwa, wamerejea nyumbani. Unadhani ni wao tu ndiyo wanatakiwa kwenda nje ya nchi? hapana,hata wewe pia.

Tunachokiweza wengi ni kuangalia mwenzio kafungua genge la kuuza nyanya hapa, na wewe kwenda kufungua mbele yake. Mmoja akianza kuuza chai na vitumbua hapa, na wewe unaanza biashara hiyo hiyo tena unapunguza na bei ya chai yako!

Suala la kuwa na uzoefu na ujuzi kwenye soka ni jambo moja, suala la kuwa mzalendo na moyo wa kulipigania taifa lako ni jambo lingine tofauti. Timu ya taifa ya Ivory Coast inaundwa na wachezaji wote kutoka Ulaya na nchi nyingine zilizoendelea kisoka lakini, siku zote wamekuwa ni washiriki na sio washindani kama ubora wa wachezaji wao unavyozungumza.

Sikatai, ni kweli wachezaji wanaotoka nje wapo wazalendo na hata Tanzania kwa sasa tunanufaika na huduma za Mbwana Samatta, Mwinyi Kazimoto na Thomas Ulimwengu wanaokipiga nje ya nchi, lakini ni wanasoka tu ndiyo wanatakiwa kwenda nje?

Watu wengi hawapendi kuambiwa ukweli, wanapenda kusifiwa na kuchekewa. Wanapenda kukosoa kuliko kushauri. Tangu tulipogundua kuwa shule zinazoitwa "English Medium" ndiyo dili, wakenya na waganda wengi wamepata ajira nchini kutokana na wao kumudu lugha ya kiingereza.

Mtanzania hata akisikia kuna nafasi ya kufundisha Kiswahili nchini Rwanda, hawezi kwenda ila anataka Ramadhani Singano akacheze mpira kwenye klabu ya APR! Kwa hali hii kwa nini nisiwapongeze kina Boban kwa uthubutu wao?

Tunahitaji siku moja kusikia kocha Suleiman Matola akiinoa klabu ya Gor Mahia ya nchini Kenya, Felix Minziro akiifundisha timu ya taifa ya Sudan Kusini, huku kocha Mecky Mexime akiwafundisha klabu ya Vital'O ya huko Burundi. Unadhani wanaotakiwa kwenda nje ni kina Shomari Kapombe tu?

Mapema mwaka huu chama cha soka nchini Ghana, kiliamua kutuma sehemu ya benchi lake la ufundi kwenda kuitembelea klabu ya Liverpool kule Uingereza kwa lengo la kujifunza namna timu inavyoendeshwa ili kujipanga kuelekea michuano ya kombe la dunia Brazil.
 
Pamoja na kutofanya zivuri kwenye michuano hiyo lakini naamini, kuna jambo kubwa waGhana watakuwa wamejifunza. Wakati wenzetu wakifikiri kwa kuangalia mbali zaidi, sisi bado tunamsonya Mrisho Ngassa kwa kung'ang'ania soka la bongo tu.

Unadhani anayetakiwa kwenda nje ya nchi kupata ujuzi na uzoefu ni Mrisho Ngassa tu? ....anyway, hata mimi pia natakiwa kwenda.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!