Searching...
Image and video hosting by TinyPic
24 March 2014
Monday, March 24, 2014

Moyes asubiri kwa hamu Debi ya Manchester

David Moyes @ Getty Images



David Moyes amesema Manchester United wataenda kwenye debi ya Jumanne dhidi ya Manchester City uwanjani Old Trafford wakiwa roho juu baada ya kushinda mechi mfululizo. 

United, ambao hawapiganii tena kushinda taji msimu huu baada ya msimu mbaya, walifuatiliza ushindi wao Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Olympiakos kwa ushindi wa 2-0 West Ham. 

City, ambao wanaweza kusonga hadi alama tatu pekee nyuma ya viongozi Chelsea wakishinda, waliwalaza United 4-1 uwanjani Etihad Septemba mwaka jana.
"Tutaingia kwenye mechi yetu ijayo tukiwa tumejiamini na tayari kwa ushindi,” akasema Moyes. 

United wako nyuma ya majirani wao City, ambao wako nambari tatu Ligi ya Premia, kwa alama 12, timu hiyo ya Moyes ikiwa imecheza mechi mbili zaidi. 

Debi hiyo ndiyo mechi ya kwanza ya ligi kwa United kuchezea Old Trafford tangu waaibishwe 3-0 na Liverpool 16 Machi.
Lakini United walijikwamua kutoka kwa kichapo hicho na kusonga mbele hadi robofainali Ligi ya Mabingwa kwa kufuta kichapo cha 2-0 mechi ya kwanza dhidi ya mabingwa wa Ugiriki Olympiakos na kisha wakashinda kwa urahisi wakiwa West Ham. 

Wayne Rooney alifunga mabao yote mawili wakiwa Upton Park, bao la kwanza likiwa kombora la ajabu kutoka nusu ya West Ham ambalo limebunisha shuti linalokumbukwa sana la David Beckham kutoka katikati ya uwanja akichezea United dhidi ya Wimbledon mwaka 1996. 

"Kwa Wayne kugundua kwamba kipa alikuwa ametoka eneo lake alipopewa mpira, ulikuwa ujuzi wa kipekee na alivyotwanga mpira pia ni kwa njia ya kupendeza sana,” akaongeza Moyes.
“Ninafikiri kila mmoja alikumbuka bao la Beckham. Yanafanana kiasi. 

“Tulicheza vizuri sana dhidi ya West Ham na jambo pekee la kutuvunja moyo ni kwamba hatukufunga mabao zaidi.”
Bao la pili la Rooney lilimfanya mchezaji huyo wa miaka 28 kuwa wa tatu kwa ufungaji mabao katika historia ya United akiwa na mabao 212, nyuma ya Sir Bobby Charlton (249) na Denis Law (237). 

Lakini alisema bao lake la kwanza dhidi ya West Ham si kali sana likilinganishwa na kiki ya kupindulia angani ambayo alifunga dhidi ya City Februari 2011. 

"Lilikuwa bao zuri na lilituweka mbele 1-0,” alisema kuhusu bao hilo lake la kwanza kutoka nje ya nusu ya uwanja ya West Ham.
"Nakumbuka bao hilo la Beckham, ni moja ya mabao makuu katika historia ya Ligi ya Premia. 

“Lilikuwa kombora kali lakini hayo ni mabao mawili tofauti. Lake alilitua ardhini, langu nilitua hewani.”
Kuhusu debi ijayo dhidi ya City, Rooney aliongeza: “Ni mechi ya kusisimua na tunatumai kwamba tutashinda.”

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!