MIAKA 10 YA KIFO CHA MARC VIVIEN FOE PART 1: SERIKALI YA CAMEROON YAWAKERA WANANCHI KWA KUAHIRISHA MAADHIMISHO KUPISHA MKUTANO WA KISIASA
Tarehe 26 mwezi Juni mwaka 2013, ilitimia miaka kumi tangu kufariki kwa mchezaji wa Kimataifa wa Cameroon Marc Vivien Foe, aliyeanguka uwanjani wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FIFA la Mabara mwaka 2003 nchini Ufaransa.
Serikali ya Cameroon hata hivyo iliahirisha shughuli kubwa iliyoandaliwa kwa ajili ya kumbukumbu ya kifo chake, hatua ambayo imezua malalamiko ya wananchi wengi wanaodai kupuuzwa kwa mchezaji huyo.
Amekuwa ni mtu mwenye kuenziwa kwa kiwango cha juu kuanzia FIFA hadi vilabu alivyovitumikia wakati wa uhai wake hususani timu za Olympic Lyon, West Ham United na Manchester City.Kifo cha Foe kiliamsha taharuki kubwa Duniani hasa kwa kuzingatia kilitokea kwenye michuano mikubwa na wakati ambapo Cameroon ilikuwa na mashabiki lukuki kutokana na ubora wa timu yao.
Serikali ya Cameroon ilipanga maadhimisho makubwa ya kumkumbuka Foe akitimiza miaka kumi kaburini hivi leo na maandalizi yote yalikwisha kamilika, lakini imeahirisha na kusogeza mbele hadi mwezi ujao kwa ajili ya kupisha Mkutano Mkuu wa Marais na Wakuu wa Nchi za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati ulioanza jumatatu wiki hii Jijini Yaunde.
Wananchi wa nchi hiyo wameghadhibishwa na kitendo hicho na baadhi yao wamenukuliwa wakisema kuwa Rais Paul Biya na Serikali yake wameshindwa kuonyesha heshima inayomstahili marehemu Foe. Taarifa ya Serikali imesema kuwa Imeandaa shughuli hiyo kwa wiki nzima kuanzia Julai 20 hadi 27 itakayofanyika kwenye kituo kilichopewa jina la mchezaji huyo katika eneo la Nkomo-Okoui, Jijini Yaunde.
Marc Vivien Foe alikufa kutokana na mshituko wa moyo katika mchezo dhidi ya Colombia na kifo chake kimechukuliwa kama fundisho kwa wadau wa mpira wa miguu duniani kuhakiki afya za wachezaji na hasa vipimo vya moyo kila wakati.
Jambo hilo bado linasugua vichwa vya watafiti wa afya na bado hakuna majibu ya moja kwa moja ya kwa nini wachezaji wanakufa viwanjani kwa matatizo ya moyo ilhali wanapimwa afya zao ipasavyo. Wengi bado wanakumbuka mkasa uliompata mchezaji wa ligi kuu ya England Fabrice Muamba aliyezimia kwa siku kadhaa baada ya kuanguka uwanjani kutokana na matatizo ya moyo, Muamba alisalimika na amejiuzulu kucheza mpira kabisa licha ya umri wake mdogo wa miaka 23.
Rekodi zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2003 wanasoka 38 wamekufa viwanjani kutokana na kutatizwa na moyo akiwemo Alen Pamic wa Croatia aliyekufa Ijumaa ya wiki iliyopita baada ya moyo wake kusimama ghafla.
Jamii ya wapenda soka duniani imeendelea kumkumbuka na kumuenzi Foe kwa matukio mbalimbali na mwezi Mei mwaka huu, Mchezaji wa Kimataifa wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang alishinda tuzo ya Marc Vivien Foe inayotolewa kwa mchezaji bora kutoka Afrika miongoni mwa ambao wanacheza ligi kuu ya Ufaransa.
Barabara jirani na ulipo uwanja alipofia Stade de Gerland mjini Lyon imepewa jina lake wakati mjini Lens huko huko Ufaransa Mtaa unaolekea uwanja mkubwa wa soka Stade Bollaert umebatizwa jina lake pia. Kadhalika kwenye uwanja wa City of Manchester umejengwa mnara mdogo kwa ajili ya kumbukumbu yake.
Kijana mmoja mjini Garoua nchini Cameroon ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa Simba huwa hafi bali anasinzia tu, akimaanisha kwamba Wacameroon bado wapo na kipenzi chao Marc Vivien Foe wanayeamini kuwa amesinzia tu.
0 comments:
Post a Comment