Searching...
Image and video hosting by TinyPic
2 April 2014
Wednesday, April 02, 2014

NIONAVYO MIMI:UZEE MWISHO NI GETINI PALE OLD TRAFFORD.



Na Oscar Oscar Jr
+255789784858

Kuna nadharia nyingi zinazobainisha hatua mbali mbali za makuzi ya mwanadamu na wataalamu wanatofautiana.Wapo wanaosema kuna hatua sita,wapo wanaosema ziko nane lakini,kundi kubwa,linabainisha hatua kuu nne ambazo binadamu anapitia.Kuna kipindi cha utoto,Kipindi cha ujana,kipindi cha utu uzima na mwisho,hatua ya uzee.Katika vipindi vyote hivi kuna mazuri na mabaya yake lakini,kipindi cha ujana ndiyo hatua ambayo wengi wangependa kubakia hapo milele!

Wapo watu wazima ambao hata salama yetu ya "shikamoo" wakipewa na mtoto wa shule,wanachukia na kuitikia kwa karaha! unabaki unajiuliza,hivi wewe si umeshavuka miaka 45? mbona sasa unakataa salamu inayokufaa? ujana una mambo mengi sana,ni kipindi ambacho mtu anakuwa hana majukumu,yuko huru kufanya chochote,ni kipindi ambacho unaona kama dunia yote iko mfukoni mwako.Asikuambie mtu,hakuna mtu ambaye angependa kutoka kwenye hatua hii!

Unapofikia utu uzima,uhuru unapungua na kuna vitu unalazimika kufanya hata kama hupendi.Mavazi utalazimika kubadilisha,mwendo,namna ya kuzungumza,kila kitu utabadilika.Ulikuwa unakwenda Bar kujiachia,kwa sasa unanywea tu nyumbani.Ukitaka kucheza muziki,inabidi ujifungie chumbani maana ukienda Club,utakutana na binti zako! kutokana na hali hii,ndiyo maana wanaoupenda ujana,wanakwambia,uzee mwisho Chalinze,mjini kila mtu anaitwa baby!

Umri ni moja kati ya vigezo muhimu sana kwenye mchezo wa soka kwa sababu,mchezo huu unahitaji zaidi nguvu.Hivi karibuni kocha wa chelsea Jose Mourinho alikuwa akilalamika kuwa,ukosefu wa makali ya Samwel Eto'o ni kwa sababu ya umri wake ambao alisema huenda ni miaka 35 badala ya ile 32 inayojulikana.

Pamoja na kuwa umri ni kigezo lakini,kwenye soka la kisasa,watu wanazingatia zaidi kile mchezaji anachofanya uwanjani na sio umri uliondikwa kwenye vyeti.Frank Lampard pamoja na umri wake wa mika 35,tangu atoke Westham United na kujiunga na Chelsea,kila msimu anafunga goli zaidi ya 10.John Terry na miaka yake 33,ni moja kati ya mabeki bora wa EPL msimu huu.Upande wa pili,ukimuangalia mtu kama Pirlo,Thomas Rosicky,Didier Drogba hawa wote,sio kina "baby" lakini,bado wanaendelea kufanya mambo ingawa sio kwa kiwango kile cha miaka minne ya nyuma.

Jana ilipigwa mechi pale Old Trafford,Man United dhidi ya Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich,mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.Nemanja Vidic ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipa uongozi United kutokana na mpira wa kona iliyochongwa na Rooney.Baada ya dakika chache,Bastian Schweinstiger alisawazisha bao hilo baada ya kupokea mpira wa kichwa kutoka kwa Mario Manduzikic,mpaka dk 90,matokeo ni bao 1-1.

Man United waliingia kwenye mechi tayari wakiwa wameshafungwa kabla hata ya mchezo wenyewe kuanza kutokana na msimu mbovu walionao,na ubora wa mpinzani wao ambao walipewa nafasi kubwa sana ya kuisambaratisha United.David Moyes pamoja na kuwa kwenye presha kubwa,jana naweza kusema aliweza kuwa bora kwenye uteuzi wa kikosi chake cha kwanza kuliko hata Pep Gaudiola.

Moyes alichagua timu kiufundi sana kutokana na mahitaji ya wapinzani wao na wachezaji hao,hawakumuangusha.Phil Jones na Valencia upande wa kulia,lengo ilikuwa na kusaidiana kumkaba Frank Ribery na kushoto,alimuamini Buttner na kumpa mtu mzima Giggs naye amsaidie kumpunguza Arjen Roben kasi.Pep Gaudiola alitakiwa kuchagua mtu mmoja wa kuanza mechi ya jana kati ya Thomas Muller au Ton Kroos ili,Mandzukic aweze kuanza kama mshambuliaji.

United walikuwa na nidhamu ya mchezo kuliko kawaida.Walikubali kupelekwa kila upande na Bayern,lakini waliendelea kuwa watulivu hasa Michael Carrick,Rio Ferdinand na Nemanja Vidic.Rio ana umri wa miaka 35,Vidic 33 na Carrick ana 32,ukijumlisha umri wao,wanafikia karne moja(miaka 100).Kucheza dakika zote 90 huku kazi ikiwa ni kumkaba Arjen Roben,Frank Ribery na Ton Kroos,sio kitu kidogo na ndiyo maana nadiriki kusema kuwa,uzee wao waliuacha nje ya geti la Old Trafford,walipotuwa uwanjani,kila mmoja alikuwa baby.

Bado David Moyes aliendelea kwenda sambamba na kasi ya mchezo,alifanya mabadiliko ya watu sahihi na kwenye muda muafaka.Baada ya Giggs kuumia,alimleta Kagawa,Ashley Young akaingia alipotoka Buttner na Hernandez akampokea,Welback.Kama Giggs asingeumia,nadhani Fellain ndiyo alitakiwa kupumzika kwa sababu,alishindwa kucheza hata mipira ya juu ambayo ndiyo saize yake na pili,pasi zake nyingi,zilipotea.

Upande wa Pep Gaudiola siku zote huwa nasema,huyu ndiye anayeshika rimoti ya tv unapocheza naye na unakuchagulia picha ya kutazama.Baada ya kufungwa,fasta alimtoa Muller na Kroos huku nafasi zao,zikichukuliwa na Mandzukic na Mario Gotze,muda mfupi,picha la kivita likaanza na goli likarudi.Mwanaume aliyekuwa benchi,ndiye aliye kuja kutoa pasi ya goli.

Goli walilopata United,lilitaka kuwaponza.Kujiamini kulitaka kupita uwezo,walianza kujiachia kushambulia na kupoteza umakini wao katika kulinda.Hata namna goli la kusawazisha lilivyopatikana,utaona kabisa Mandzukic anaucheza mpira ule akiwa free na kuurudisha ndani kabla ya muuwaji kufanya mambo.Lahm alikuwa vizuri sana sehemu ya kiungo na kama,ndiyo unamtazama kwa mara ya kwanza,ni vigumu kujua kuwa jamaa ni fundi wa beki zote za pembeni.

Najua kule Allianz Arena,Gaudiola atakuja tofauti kabisa na alivyokuwa  jana ingawa kumkosa Bastian Schweinstiger,Thiago Alcantara na Javi Martinez kuna weza kumuathiri.Ni rahisi kuziba pengo la Martinez kwa sababu,Dante yupo lakini,ni vigumu sana kuziba pengo la Schweinstiger.Bastian ndiyo chuma "original" cha kijerumani,mapafu ya mbwa,roho mbaya,mafia,ninja kumkosa ni pigo kwa Pep Gaudiola.

United jana walikuwa hawana tofauti na mume na mke waliogombana,halafu,wakamaliza tofauti zao.Hapa si mmeshanielewa? au mpaka niseme watafanya nini siku hiyo? Mashabiki zaidi ya elfu 70 akiwemo Sir Alex Ferguson,walikuwa wanamsapoti David Moyes na timu kwa dakika zote 90.Huwezi kuamini kama kuna kikundi cha "wahuni" kilikodisha ndege hivi karibuni na kupeperusha bango la kushinikiza Moyes atimuliwe,wote waliungana na kuwa kitu kimoja.

Bado mechi ya marudiano sio rahisi kwa pande zote mbili,hasa upande wa united kwa sababu,ukichunguza takwimu za jana,utaona kuwa Bayern walitawala karibu kila idara ingawa,kwenye soka hakuna kinachoshindikana.Kama United watafanikiwa kumuondoa Bayern na kutinga hatua ya nusu fainali,sintoshangaa kuona msimu ujao wakicheza michuano hii ya klabu bingwa kwa nafasi ya bingwa mtetezi.Kama unaweza kumfunga Bayern na kusonga mbele,ni wazi pia kuwa,unaweza kumfunga mbabe mwingine yoyote.

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali,ukichanganya umri wa Michael Carrick,Rio Ferdinand na Nemanja Vidic,unapata karne moja (miaka 100) ambayo ipo katika kundi la uzee.Kilichofanyika jana,hawa wote waliacha uzee wao pale getini Old Trafford na walipotua uwanjani,kila mtu alikuwa baby.

Leo naishia hapa,naomba kutoa hoja.Kama unachochote na ungependa kushirikiana na mimi,unaweza kunitafuta kwenye ukurasa wangu wa Facebook au ukachat na mimi  kwa whatsapp kwenye namba +255789784858

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!