Searching...
Image and video hosting by TinyPic
7 February 2015
Saturday, February 07, 2015

Uchambuzi: Everton vs Liverpool


Na Oscar Oscar Jr

Mechi ya mwisho ya watani wa Jadi kwa Nahodha Steven Gerrard ndani ya Jiji la Liverpool, itapigwa leo ndani ya dimba la Gordison Park ambapo Liverpool watakuwa ugenini kuvaana na ndugu zao wa Everton.

Everton msimu huu wamepungua ubora na moja ya sababu za hali hiyo ni kuukosa muunganiko wa kiungo James Mccarthy na Gareth Barry ambao walicheza vizuri sana msimu uliopita. 

Kukosekana kwa Maccarthy, kumetoa nafasi ya Mohamed Besic ambaye anaonekana kuanza kuelewana na Barry na leo watakuwa na mtihani wa kuwazuia Steven Gerrard na Raheem Sterling ambao wanaweza kuanza kwenye eneo la ushambuliaji.

Tangu kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alipobadili mfumo na kutumia 3-4-2-1 timu imeonekana kuimarika huku Lucas Leiva akicheza sambamba na Jordan Hernderson kwenye eneo la kiungo mbele ya mabaeki watatu na kuifanya ngome kuwa imara zaidi.

Romeru Lukaku ni moja kati ya wachezaji wenye rekodi ya kufunga magoli kwenye Derby hii kwa siku za hizi karibuni na kunauwezekano nyuma yake akaanza kiungo mshambuliaji, Ross Barkley.

Barkley  kabla ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu, wengi walikuwa wanamtaja kama moja ya wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu EPL leo hii upo uwezekano wa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.

Liverpool ambao wanakamata nafasi ya saba wakiwa na pointi 38, wameonekana kuimarika zaidi hasa baada ya kipa, Simon Mignolet kuonyesha kiwango bora na kuacha makosa madogo madogo ambayo yalikuwa yanaigharimu timu kwa muda mrefu.

Pamoja na kuwa Everton wanakamata nafasi ya 12 huku wakiwa wamefungwa mabao 34, leo hii watakuwa na kiu ya kupata ushindi ili wazidi kujiweka kwenye mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi kuu hasa ukizingatia kuwa, tofauti yao na Leicester City wanaokamata mkia ni alama tisa pekee.

Leighton Baines ni moja kati ya wachezaji waliochangia mabao mengi ya Everton msimu huu kutokana na pasi zake za mwisho na leo kama Emre Can ataanza kama beki wa kulia, atalazimika kuwa kwenye ubora wa hali ya juu ili kutomruhusu Baines kushambuliaji akitokea pembeni.

Derby hii imekuwa ikizalisha mabao mengi na mara ya mwisho timu hizi zilipokutana Gordison Park kwenye mchezo wa ligi kuu, mabao sita yalifungwa huku timu zikitoka sare ya 3-3. 

Ubora wa sasa wa Liverpool unafanya wapewe nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi ingawa mchezo huu huwa haujalishi nani yuko chini kwenye msimamo katika kumpata mshindi ndani ya dakika 90.

0 comments:

Post a Comment

 
Back to top!